Aprili 2016


Mheshimiwa Rais,

Kwanza tunakupongeza kwa kasi uliyoanza nayo tangu kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania.

Kama unavyofahamu Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la ujangili wa Tembo, huku ikiwa imepoteza zaidi ya nusu ya idadi ya Tembo ndani ya miaka mitano. Tembo ni mnyama ambaye ni kivutio namba moja katika safari za Utalii barani Africa. Kupotea kwa mnyama huyu kunaathiri moja kwa moja idadi ya watalii ambayo inakuja kutembelea maliasili zetu. Kupitia utalii, tembo hai ana thamani mara sabini na sita zaidi ya meno ya Tembo aliyekufa .

Okoa Tembo wa Tanzania ni Kampeni ya Watanzania wanaojali kwa ajili ya Tembo wa Tanzania. Kampeni ina wafuatiliaji zaidi ya 100,000 (Laki moja) kwenye Facebook, tangu imeanza mwezi wa nane 2015. Kampeni hii ina malengo matatu ambayo yanatoa wito kwa serikali ya Tanzania kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo pasipo kujali utaifa, hadhi au mamlaka, na kutumia urafiki wa Kihistoria kati ya Tanzania na China kufunga masoko ya meno ya Tembo huko China.

Kwa barua hii, tunaomba utekelezaji wa mara moja wa lengo la tatu la kampeni hii ambalo ni: Kuteketeza hadharani ghala la meno ya Tembo Tanzania – linalosadikika kuwa kubwa kuliko yote ulimwenguni.

Kwa masikitiko makubwa, tumesoma kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii ya mwezi Machi 2016, kuwa Tanzania haitaharibu ghala lake la meno ya Tembo. Tunaamini kuwa hili ni kosa kubwa kwa nchi yetu, na tunaomba ulitazame upya. Sababu kuu tunayoisikia kukataa kuharibu ghala hilo ni kuwa upo uwezekano wa kuuza ili kupata fedha za uhifadhi, lakini mjadala huu unawaweka Tembo wetu hatarini.

Kutokana na kufungwa na mkataba wa kimataifa wa biashara juu ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka (Convention on International Trade in Endangered Species – CITES), Tanzania kwa sasa haiwezi kuuza ghala lake la meno ya Tembo. Mwaka 2014 Tanzania ilisaini mpango wa kuwalinda Tembo (Elephant Protection Initiative) uliozuia uuzaji wa meno ya Tembo kwa muda wa miaka kumi. Vilevile nchi wanachama wa CITES haziruhusiwi kuuza meno ya Tembo yaliyokamatwa kutokana na ujangili.

Hata hivyo, uwepo wa ghala hili la meno ya Tembo unawapa moyo wafanyabiashara haramu wa meno ya Tembo kuwa biashara itaendelea tena. Uuzaji wa meno ya Tembo hauendani na usitishaji wa biashara ya meno ya Tembo. Zipo nchi zilizowahi kuruhusiwa kuuza maghala yake kwa China na Japan mwaka 2008; miongoni mwao ni Botswana, Namibia na Afrika Kusini. Historia inaonyesha kuwa mauzo ya maghala yaliyopita yalichochea biashara haramu ya meno ya Tembo, na biashara hii ndio sababu kubwa inayochochea ujangili hivyo kuwaweka Tembo wetu hatarini. Mauzo ya ghala la meno ya Tembo yanaweza kuathiri mapato hayo aidha kwa vikwazo vya utalii au kuchochea ujangili zaidi. Fedha nyingine nyingi zinaweza kupatikana kwa kupitia utalii wa wanyamapori, chanzo cha mapato ambacho kinakua, kinajitosheleza na kina manufaa kwa Watanzania wengi na kwa muda mrefu.

Hata China na Hong Kong, mahali ambapo kuna masoko makubwa ya meno ya Tembo, wametambua kuwa hakutakuwa na usalama wa Tembo kama biashara ya meno ya Tembo itaendelea, wao pamoja na Marekani Mwaka 2015 waliweka azma ya kufunga masoko ya ndani. Pia nchi nyingine kama Ufilipino na Thailand zimeanza kuharibu ghala zao za meno ya Tembo. Kama Tanzania inaendelea kutunza ghala lake, ni nani anayefikiriwa kuwa mteja wake hapo baadaye? Ni kwa kufunga tu biashara ya meno ya Tembo kimataifa ndiko kunakoweza kuwaokoa Tembo wetu milele.

Hatimaye ushawishi unaanza kukua ulimwengunikwa hatuahii ya Kihistoria.Kuharibu ghala la meno ya Tembo kunatuma ujumbe mzito kwa majangili na wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani ya pesa, na kuwa ujangili ni kosa la jinai lisilokubalika. Nchi nyingi za Afrika kama Kenya, Ethiopia, Chad, Gabon, Mozambique na Congo zimeonyesha dhamira yao kwa kuteketeza maghala yao, walipongezwa sana kimataifa kwa kufanya hivyo na iliongeza ufadhili wa wahisani kwa uhifadhi na kupambana na ujangili.

Kenya ni miongoni mwa nchi za Africa ambazo zimetekeleza mpango huu kwa kuchoma ghala lake kwa awamu tatu, na mnamo tarehe 30 mwezi Aprili, watachoma ghala lote lililosalia. Tukio hili ni kubwa sana na limeungwa mkono kimataifa.

Tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kufuata mfano wa Serikali ya Kenya na nchi nyingine kwa kuteketeza ghala lake la meno ya Tembo. Ni muhimu kuweka rekodi ya idadi na kufanya uchambuzi wa kisayansi katika ghala la meno ya Tembo kabla ya kulichoma kwani hii itasaidia kupambana na ujangili na pia kuongeza jitihada za ufuatiliaji wa sheria. Meno ya Tembo yanapotumika kama ushahidi katika kesi mahakamani juu ya wafanyabiashara haramu wa meno ya Tembo, yanatakiwa kuchukuliwa sampuli na kuhifadhiwa, kisha kuharibiwa baada ya kesi.

Ni bora kuweka jitihada juu ya haki za wananchi kuona Tembo hai, kuliko kujikita kutunza meno ya Tembo katika makumbusho ya Taifa ambayo yanakuwa kama ushahidi wa Kitendo kiovu cha ujangili kilichopelekea upotevu wao.

Hatma  ya Tembo wetu ipo mikononi mwetu. Tuchukue hatua madhubuti kuwaokoa Tembo wetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Kwa niaba ya Watanzania zaidi ya 100,000 wanaounga mkono kampeni hii katika ukurasa wa Facebook, tunakufikia Mheshimiwa Rais kutoa wito kwako kuwaokoa Tembo wetu na kutimiza kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano “HAPA KAZI TU”.

Kwa kupokea barua hii, tunaomba kuonana na kujadili mambo tajwa hapo juu.

Tunashukuru sana

 Peter Lijualikali                  Member of Parliament and Shadow Environment Minister
Zitto Kabwe                 Member of Parliament, ACT
Vanessa Mdee            WildAid Ambassador
Millard Ayo                        Clouds Media Group
Ponjoli Joram                     Natural Resources Project Officer, Delegation of the European Union
Charles Hillary              Editor, Azam Media
Noah Mpunga              Director, WCS Southern Highlands Conservation Program
Vedasto Msungu         Environmental Journalist, ITV and Radio ONE
Wallace Maugo            Editor, The Guardian
Florence Majani                 Deputy Editor, Mwananchi Communications
Wasiwasi Mwabulambo    Programmes Manager, Azam Media
Hudson Kamoga          Journalist
Andimile Martin           Conservationist
Imani Kajula                       CEO, EAG Group
David Kabambo           Director, Peace for Conservation
Lasway Romane                Lecturer, National Institute of Tourism
Josiah Mshuda             Director, DONET
Monica Lumambo        Chairperson, KINET
Damien Kosei               Secretary-General, BAENET
Dativa Kimolo               Chairperson, DACENET
Said Mjui                       Guardian, Mtamako
Beda Kihindo                Education Officer, TALGWU
Pierre Nyakwaka          Planning Officer, Jiendeleze Trust
George Mtemahanji     CEO, Sun Sweet Solar
Arafat Mtui                    Coordinator, Udzungwa Ecological Monitoring Center
Pima Nyenga                Director, Association Mazingira
Lameck Mkuburo         Elephant Researcher, Southern Tanzania Elephant Program
Jenipha Mboya            Researcher, Southern Tanzania Elephant Program
Shubert Mwarabu         Me Against Poaching
Meyassi Meshillieck     Director, Serengeti Preservation Foundation
Abbas Mvungi              Director, Friends and Protectors of Wildlife
Mckene Ngoroma                Director, ECO Footprints TZ