Novemba 2015

Kwako Rais wa Tanzania,

Hongera kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania.

Sisi, kama wananchi wa Tanzania tunaojali, tunakuandikia leo kukuomba kuchukua hatua juu ya suala la kupungua kwa kasi idadi ya Tembo nchini, kutokana na ujangili kwa ajili ya biashara haramu ya meno ya Tembo.

Miaka hamsini iliyopita, kulikuwa na Tembo 300,000 nchini Tanzania. Mwaka 2009, kulikuwa na Tembo 109,000. Mwaka 2014, ilikadiriwa kuna Tembo 43,000 tu waliobaki – upungufu wa asilimia 60 ndani ya miaka mitano tu (Ripoti ya Sensa ya TAWIRI 2014).

Tunaomboleza kwa upotevu wa haya maelfu ya Tembo, ambao kila mmoja alikuwa na familia na marafiki, wakiishi pamoja, wakisherehekea kuzaliwa kwa Tembo wapya, na kusikitikia vifo vya wenzao.

Tunaomboleza pia namna ambavyo maelfu ya mizoga hii inaleta hasara katika Taifa letu. Tembo wanaunda sehemu muhimu ya urithi wetu wa asili. Wanashirikishwa katika hadithi zetu na sanaa zetu, inadhihirisha kuwa Binadamu na Tembo wana uhisiano wa muda mrefu. Mfumo wa ikolojia ya Afrika Mashariki ulitokea pamoja na Tembo, ukiunda mbuga na misitu ambapo njia zao zilibaki kuwa barabara zetu. Kupoteza Tembo wetu ni kupoteza sehemu muhimu ya kihistoria na alama ya Taifa letu.

Tatizo la ujangili wa Tembo pia linatishia moja ya chanzo kikubwa cha pato la Taifa letu ambacho ni utalii. Zaidi ya watu milioni moja hutembelea Hifadhi za Taifa kila mwaka, ambapo huchangia kwenye sekta ya utalii ambayo inaajiri mamia na maelfu ya watu, na inachangia asilimia 14 ya uchumi wa Taifa (WTTC 2015). Kutopenda Tembo hakumpelekei mtu kutotambua kuwa ujangili ni uhalifu na tishio kubwa kwa uchumi wa Taifa.

Tunatambua hatua zilizofanyika kukabiliana na tatizo la ujangili. Uundaji wa mikakati ya kitaifa dhidi ya ujangili, juhudi za Kikosi Kazi cha National and Transnational Serious Crimes Investigation Unit (NTSCIU), na kuongeza rasilimali kwa mamlaka yetu ya wanyamapori ni hatua muhimu. Hata hivyo ujangili utaendelea kama tutashindwa kushughulikia chanzo kikubwa cha ujangili ambacho ni biashara ya meno ya Tembo.

Pasipo kujali kiwango cha tatizo la ujangili, suala hili lina ufumbuzi wa wazi ambao serikali ya Tanzania ina nafasi ya kutekeleza. Tunatoa wito kwa serikali ya Tanzania kufanya yafuatayo:

1. Kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo nchini, bila kujali utaifa, hadhi au     mamlaka.

Kwa kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo kunaondoa motisha, vyanzo na mianya yote ya ujangili wa Tembo kwa wafanyabiashara wa ndani. Kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo kutavunja mitandao ya ujangili na kuwaondoa wengine wenye kujihusisha na biashara haramu ya meno ya Tembo.

2. Kutumia urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na China kufunga masoko ya meno ya Tembo huko China.

Takribani asilimia 90 ya meno ya Tembo toka Tanzania yanauzwa China, ambapo biashara halali ya meno ya Tembo inatumika kama mwavuli wa biashara haramu ya meno ya Tembo ambacho ndio chanzo kikuu cha tatizo la ujangili wa Tembo. Tunaishawishi serikali ya Tanzania kuiomba China kutekeleza ahadi yao ya kufunga masoko yote ya meno ya Tembo milele, ili kuweza kulinda usalama wa muda mrefu wa Tembo. Kama mtumiaji mkubwa wa meno ya Tembo, kufunga biashara China kungepelekea kuanguka kwa haraka kwa biashara ya meno ya Tembo kwa sehemu nyingine ulimwenguni.

3. Kuteketeza hadharani ghala ya meno ya Tembo Tanzania – inayosadikika kuwa kubwa kuliko yote ulimwenguni.

Kutokana na kufungwa kwa mkataba wa kimataifa wa biashara juu ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka (Convention on International Trade in Endangered Species – CITES), Tanzania kwa sasa haiwezi kuuza ghala yake ya meno ya Tembo. Mwaka 2014 Tanzania ilisaini mpango wa kuwalinda Tembo (Elephant Protection Initiative) uliozuia uuzaji wa meno ya Tembo kwa muda wa miaka kumi. Hata hivyo, uwepo wa ghala hili la meno ya Tembo linawapa moyo wafanyabiashara haramu wa meno ya Tembo kuwa biashara itaendelea tena. Uuzaji wa meno ya Tembo hauendani na usitishaji wa biashara ya meno ya Tembo, na mauzo yaliyopita ya maghala yalichochea biashara haramu ya meno ya Tembo. Kuharibu ghala la meno ya Tembo kunatuma ujumbe mzito kwa majangili na wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani ya pesa, na kuwa ujangili ni kosa la jinai lisilokubalika.

Ni gharama kutunza na kulinda ghala la meno ya Tembo Tanzania. Nchi nyingi za Afrika zimeonyesha dhamira yao kwa kuteketeza maghala yao. Walipongezwa sana kimataifa kwa kufanya hivyo, na iliongeza ufadhili wa wahisani kwa uhifadhi na kupambana na ujangili. Fedha nyingine nyingi zinaweza kupatikana kwa kupitia utalii wa wanyamapori, chanzo cha mapato ambacho kinakua kinajitosheleza na kina manufaa kwa Watanzania wengi kwa muda mrefu, kuliko kuuza mara moja tu ghala la meno ya Tembo ambako kunaweza kuchochea ujangili zaidi na kupelekea upotevu wa Tembo wa Tanzania.

---

Nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa Tembo hapo kabla. Mwaka 1989, Tanzania iliongoza jitihada za kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo ulimwenguni – tulipochukua hatua kukomesha mauaji ya Tembo, dunia nzima ilituunga mkono. Ni lazima turejeshe upya dhamira yetu kwa ahadi tuliyojiwekea kwa hatua ya kimataifa zaidi ya miaka ishirini iliyopita, na kuleta ukomo wa biashara yote ya meno ya Tembo.

Rekodi ya Tanzania juu ya uhifadhi wa Tembo sio suala la mtazamo wa kimataifa tu, bali pia ni suala la wananchi wa Tanzania. Zaidi ya watu 50,000 wameunga mkono kampeni ya 'OKOA Tembo wa Tanzania' kwenye Facebook. Kwa niaba ya wananchi wa Tanzania tunakufikia, mheshimiwa Rais, kutoa wito kwako kuwaokoa Tembo wetu.

Kuleta amani kwa Tembo wa Tanzania na maeneo yake ya hifadhi, na kulinda sekta ya utalii ya wanyamapori ambayo ni faida kwa Watanzania wote – hii inaweza kuwa ukumbusho kwako.

Kwa utiifu,

 1. Benson Kibonde                      Mhifadhi Selous Game Reserve, Idara ya Wanyamapori
 2. Prof. J.R. Kideghesho              Department of Wildlife Management, Sokoine University of Agriculture
 3. Prof. B.M. Mutayoba                Faculty of Veterinary Medicine, Sokoine University of Agriculture
 4. Prof. C. Nahonyo                     Department of Zoology and Wildlife Conservation, University of Dar es Salaam
 5. Vanessa Mdee                        WildAid Ambassador
 6. Millard Ayo                              Mwanahabari, Clouds Media Group
 7. Lathifa K. Sykes                      CEO, Hotel Association of Tanzania (HAT)
 8. Dr. Dennis K. Ikanda               Mkurugenzi TAWIRI–KPR Centre
 9. Ponjoli Joram                          Natural Resources Project Officer, Delegation of the European Union
 10. Charles Hillary                         Mwanahabari, Azam Media
 11. Noah Mpunga                         Mkurugenzi, WCS Southern Highlands Conservation Program
 12. Vedasto Msungu                    Environmental Journalist, ITV na Radio ONE
 13. Wallace Maugo                       Mhariri, The Guardian
 14. Florence Majani                      Mhariri Msaidizi, Mwananchi Communications
 15. Wasiwasi Mwabulambo         Meneja Programu, Azam Media
 16. Imani Kajula                            CEO, EAG Group
 17. David Kabambo                      Mkurugenzi, Peace in Nature
 18. Lasway Romane                     Mhadhiri, Chuo cha Taifa cha Utalii
 19. Josiah Mshuda                       Mkurugenzi, DONET
 20. Monica Lumambo                  Mwenyekiti, KINET
 21. Damien Kosei                         Katibu Mkuu, BAENET
 22. Dativa Kimolo                         Mwenyekiti, DACENET
 23. Said Mjui                                 Mlezi, Mtamako
 24. Beda Kihindo                          Afisa Elimu, TALGWU
 25. Pierre Nyakwaka                    Afisa Mipango, Jiendeleze Trust
 26. George Mtemahani                CEO, Sun Sweet Solar
 27. Arafat Mtui                              Mratibu, Udzungwa Ecological Monitoring Center
 28. Pima Nyenga                          Mkurugenzi, Association Mazingira
 29. Lameck Mkuburo                   Mtafiti wa Tembo, Southern Tanzania Elephant Program
 30. Jenipha Mboya                       Mtafiti, Southern Tanzania Elephant Program
 31. Shubert Mwarabu                   Me Against Poaching